Gavana wa Kaunti ya Narok Patrick Ntutu, ametoa ahadi ya kuimarisha miundombinu katika eneo la Emurua Dikirr. Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, Ntutu alitangaza kuwa serikali yake imetoa kiasi cha 400,000,000 kwa wadi nne katika eneo hilo ili kushughulikia masuala ya afya, maji, barabara mbovu, na elimu.
Ntutu aliwasihi wakazi wa eneo hilo kushirikiana na serikali kuhakikisha maendeleo yanapatikana, huku akisisitiza kuwa lengo kuu la serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa serikali.
Kwa upande wake kamishna wa Kaunti ya Narok, Isaac Masinde, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, aliahidi kuchukua hatua dhidi ya wezi wa mifugo katika eneo la Transmara magharibi. Masinde alisema kuwa wezi wa mifugo wamekuwa wakiwatia wasiwasi wanajamii katika eneo hilo na kusababisha kudorora kwa usalama, sio tu katika eneo la Transmara bali pia katika kaunti jirani ya Migori.
In the company of Narok County Commissioner, I have arrived at Emurua Dikirr Primary School, Ilkerin Ward, Emurua Dikirr Constituency for this year’s Mashujaa Day celebrations. pic.twitter.com/Nviy5etBCn
— Governor Patrick Ole Ntutu (@OleNtutuK) October 20, 2023
Wakati hayo yakijiri wabunge kutoka katika maeneobunge ya Narok Kaskazini, Narok Kusini na Emurua Dikirr katika kaunti hii ya Narok, wameahidi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Gavana Patric Ntutu katika jitihada zake za kuinua hadhi ya Kaunti ya Narok na kuendelea kuleta miradi ya maendeleo.
Wakizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Mashujaa wabunge hao wakiongozwa na mwenyeji wao Johana Ngeno, Mbunge wa Narok kusini Kitilai Ntutu, Agnes Pareiyo wa Narok Kaskazini na mbunge mwakilishi wa kike katika kaunti ya Narok, wameshabikia hatua ya kulipwa fidia kwa wananchi waliofurushwa kutoka kwenye arthi ya msitu wa Mau. Wabunge hao wamesema kwamba fedha hizo zitawawezesha kuendeleza maisha yao kwa urahisi.