Serikali ya Taifa la Sudan imemwagizwa Balozi wake Nchini Kenya kuondoka humu nchini mara moja, kufuatia mkutano wa Rais William Ruto na Kiongozi wa vuguvugu la RSF jijini Nairobi siku ya Jumatano.

Katika taarifa iliyotolewa na Shirika la Taifa la Habari nchini Sudan (SUNA) Alhamisi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali al-Sadiq, alieleza kwamba balozi huyo ameitwa nyumbani kwa mashauriano, huku akilaani mapokezi rasmi yaliyoandaliwa na Serikali ya Kenya kwa kiongozi wa RSF. Waziri huyo aliongeza kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri mahusiano ya Kenya na Sudan katika siku za usoni.

Kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, amekuwa katika ziara ya kikanda, akitembelea nchi mbalimbali kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo kati ya RSF na vikosi vya serikali vya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan. Sudan ilikuwa imewaonya wa nchi zinazomkaribisha kiongozi huyo wa RSF kwamba watakuwa washirika wa mauaji ya wananchi nchini Sudan.

Dagalo tayari ameyatembelea mataifa ya Uganda, Ethiopia, Djibouti, na Kenya na kwa sasa, yuko nchini Afrika Kusini.

 

January 5, 2024