Mafisa wa polisi katika eneo la Suswa, Narok Mashariki, wamepewa hadi siku tano kuhama baada ya makabiliano makali kati yao na waandamanaji, yaliyosababisha vifo vya watu wawili na kujeruhiwa kwa maafisa tisa wa polisi . Ghasia hizo zilichochewa na ajali ambapo kondoo 39 waligongwa na gari katika eneo la Duka Moja, Suswa.
Akihutubia wakazi wa Suswa, Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ntutu, alieleza kuwa jamii ya eneo hilo haina imani tena na maafisa wa usalama. Alitoa wito kwa serikali, kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kuwa maafisa hao wamehamishwa mara moja kutoka vituo mbalimbali nchini.
“Tangu nizaliwe, sijawahi kusikia afisa ambaye hataki kwenda uhamishoni. Ni nini hiki maalum ambacho wananufaika nacho Narok ambacho hawataki kuhama,” alisema Ntutu.
Kauli yake iliungwa mkono na wakazi wa Suswa, ambao walionyesha mshangao kuhusu hatua ya maafisa wa polisi kupinga kuhamishwa kwao. Saruni Reson, mmoja wa viongozi wa eneo hilo, alisisitiza kuwa wananchi hawataruhusu ucheleweshaji wa utekelezaji wa agizo hilo.
Aidha, Alfred Keriolale alilaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na maafisa wa polisi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakidai haki. Alikosoa hatua ya polisi kutumia silaha za moto kinyume na sheria, akisema ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mwanaharakati Memba Charo aliwasilisha ombi la kupinga uhalali wa uhamisho wa polisi hao kiholela. Charo alieleza kuwa uhamisho huo ni ukiukaji wa Kanuni za kazi.
Jaji Nduma Nderi, mnamo Jumanne, Januari 28, aliamuru Huduma ya polisi nchini NPS na Wizara ya Mambo ya Ndani kuanzisha itifaki sahihi ya uhamisho na kuwalipa maafisa hao marupurupu yao kabla ya kuanza uhamisho.