Mamlaka ya Usafiri wa Ndege nchini Tanzania (TCAA) imetangaza uamuzi wa kusitisha rasmi safari zote za abiria za Shirika la Ndege la Kenya Airways kutoka Jijini Nairobi kuelekea Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na TCAA saa kumi na moja jioni, mamlaka hiyo imesema kuwa uamuzi wa kusitisha safari za Kenya Airways ni hatua ya kulipiza kisasi kutokana na Kenya kukataa kuidhinisha shirika la Ndege za mizigo la Tanzania idhini ya kutua jijini Nairobi. Kulingana na TCAA, marufuku hiyo itaanza kutekelezwa tarehe 22 mwezi huu wa Januari.
Mzozo kati ya Tanzania na Kenya kuhusu masuala ya usafiri wa anga umeendelea kwa muda sasa. Mnamo Agosti 2020, Tanzania iliwahi kupiga marufuku safari za ndege za Kenya Airways kwa muda mfupi, baada ya Kenya kuwaondoa Watanzania katika orodha ya nchi ambao raia wake wangeweza kuingia Kenya bila vikwazo vya karantini. Ingawa marufuku hiyo iliondolewa baadaye, wasiwasi umeendelea kushuhudiwa kati ya mataifa haya mawili.