Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano NCIC imetaka kusitishwa kwa maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali yaliyoitishwa na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia amesema maandamano hayo yanazua hali ya wasiwasi kote nchini, akitoa mfano wa kisa cha Jumatatu ambapo watu waliuawa, kujeruhiwa na mali kuharibiwa.

Alikashifu uharibifu wa magari, majengo ya biashara, makanisa na misikiti katika sehemu za nchi kama vile Nairobi na Kisumu.

Kobia pia alilaani uvamizi dhidi ya ardhi ya familia ya rais wa zamani Uhuru Kenyatta ambapo kondoo wengi waliibwa, miti kukatwa na baadaye sehemu ya mali hiyo kuteketezwa.

Hata hivyo ametoa wito kwa Rais William Ruto na Bw Odinga kuketi na kutatua masuala yao.

March 28, 2023