Wanachama wa chama cha UDA katika kaunti ya Narok wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa wawakilishi mbalimbali wa chama hicho mashinani. Uchaguzi huo wa mashinani unatarajiwa kufanyika katika vituo mbalimbali kati ya saa tatu asubuhi na saa tisa alasiri.
Kivutio kikuu cha uchaguzi huu ni kinyang’anyiro cha uwenyekiti wa chama cha UDA katika kaunti, ambapo gavana wa Kaunti ya Narok Patrick Ntutu, na mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoyo, wanashindana vikali kwa nafasi hiyo.
Wito wa Amani
Wakati haya yakijiri, kamishna wa Kaunti ya Narok, Reuben Kipkech Lotiatia, ametoa wito kwa wahusika wote katika uchaguzi huo kuendeleza shughuli zao kwa amani. Akizungumza mjini Narok, Kamishna Lotiatia amesisitiza kwamba hakutakuwa na nafasi kwa watu wanaotaka kuleta fujo ili kuvuruga zoezi hilo.
Lotiatia pia ametoa hakikisho kwamba vyombo vya usalama vitakuwa macho, akiahidi kwamba yeyote atakayepatikana akihusika na vurugu atachukuliwa hatua kali za kisheria. Pia, amewasihi wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama na kuwajulisha ikiwa kuna mtu yeyote anayetaka kuharibu amani.
Mbali na Narok, chaguzi za chama tawala pia zinafanyika leo katika kaunti za Nairobi, Homabay, Busia, na West Pokot. Mhandisi Anthony Mwaura, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Bodi ya Uchaguzi ya UDA, alithibitisha kwamba maandalizi yote kuelekea uchaguzi huo yamekamilika.