Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mlipuko wa kipindupindu nchini Haiti unaenea kwa kasi, huku idadi ya maambukizi ikiongezeka maradufu na kufikia wananchi wapatao 2,000 katika muda wa siku chache zilizopita.
Wizara ya afya nchini Haiti imeripoti angalau vifo 41 kati ya Oktoba 19 na 23 mwaka huu, huku idadi ya maambukizi ikiongezeka kutoka 964 hadi 1,972. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, karibu nusu ya visa hivyo vinawajumuisha watoto walio chini ya umri wa miaka 14.
Mlipuko huo mpya wa kipindupindu ulioanza mapema mwezi huu, unatokea miaka mitatu baada ya taifa hilo maskini la Caribbean ambalo pia linakabiliana na ukosefu wa usalama, kufanikiwa kukomesha mlipuko ulioanza mwaka 2010 na kuua zaidi ya watu 10,000.