Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema kuwa uharibifu uliotokea katika barabara ya express way unaweza kuwa zaidi ya Ksh.706.7 milioni ambayo ni sawa na dola milioni 5.
Hii ni baada ya waandamanaji kung’oa ua na kuharibu barabara hapo jana wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.
Murkomen, akizungumza wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo alisema kuwa, pamoja na uharibifu wa Barabara ya Expressway, vituo vitatu vya reli na miundomsingi mingine muhimu iliharibiwa huku waandamanaji wakilenga bidhaa zinazoweza kuuzwa.
Waziri huyo amefichua kuwa uchunguzi unaoendelea tayari umefanikisha kukamatwa kwa zaidi ya watu 50, na wengine zaidi wanatarajiwa kukamatwa kwa sababu mashirika ya kijasusi yatatumia habari kutoka kwa picha za CCTV kuwatambua washukiwa hao.