Kinara wa Upinzani nchini Raila Odinga, ametoa amemsuta na kumlenga kwa vijembe Balozi wa Marekani nchini, Meg Whitman, kwa madai ya kuingilia masuala ya ndani ya Kenya na hasa kuonekana kuegemea upande wa serikali.
Akizungumza katika siku ya tatu ya kongamano la ugatuzi linaloendelea mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, Bwana Odinga amesisitiza kwamba Kenya ni taifa huru lenye katiba inayoiwezesha kujiamulia mambo yake bila kutegemea ushauri wa nje. Waziri mkuu huyo wa zamani, pia ameonyesha kukerwa na taarifa za Balozi Whitman, hususan kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita.Kauli hii ya Odinga imekuja wakati ambapo mazungumzo ya pande mbili kati ya serikali na upinzani yanaendelea.
Balozi Meg Whitman katika kikao hicho cha Ugatuzi hapo jana, alitoa hotuba ya kusifu demokrasia ya Kenya na kuelezea kuwa uchaguzi mkuu uliopita kuwa ulikuwa huru na wa haki. Hata hivyo, kauli hii ilizua hisia tofauti miongoni mwa wanasiasa na wananchi, na kusababisha maseneta wa mrengo wa Azimio la Umoja kutoa taarifa ya pamoja wakipinga kauli ya Balozi Whitman.
Maseneta hao, chini ya uongozi wa Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, wametaka ubalozi wa Marekani nchini kujitenga na masuala ya kisiasa ya Kenya, na kueleza kwamba uongozi wa nchi umekandamiza demokrasia badala ya kuiendeleza kama ilivyodaiwa na balozi huyo.