Wakenya wamepata afueni baada ya Mahakama ya Rufaa kudinda kusitisha amri ya Mahakama Kuu iliyotangaza ada ya nyumba za bei nafuu kuwa ni kinyume cha katiba.

Katika uamuzi uliotolewa asubuhi ya leo, majaji wa Mahakama ya Rufaa Lydia Achode, John Mativo na Paul Gachoka walitaja maslahi ya umma katika suala hilo, na kusisitiza uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba Ushuru wa Nyumba uliwasilishwa bila mfumo wa kisheria.

Itakumbukwa kwamba serikali ilipendekeza wakenya kutozwa ushuru wa asilimia 1.5 utakaotumika kujenga nyumba za bei nafuu katika sehemu mbalimbali humu nchini kama njia mojawapo ya kuwezesha kila mkenya kumiliki nyumba baada ya kustaafu.

Wakati hayo yakijiri Rais William Ruto ameapa kuutekeleza ushuru huo wa nyumba licha ya kutupiliwa mbali na mahakama ya rufaa.

Akizungumza huko Meru rais Ruto amedai kuwa ako na mamlaka ya kutekeleza ushuru huo na kusema kuwa utaziba mwanya wa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

January 26, 2024