Vijana katika kaunti ya Marsabit wamehimizwa kuwa mabalozi wa Amani na kukoleza jitihada za kuhubiri amani baina ya jamii mbalimbali, kama mojawapo ya njia za kutatua mizozo ya kikabila ya mara kwa mara katika kaunti hiyo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa hazina ya maendeleo ya maeneo bunge CDF katika eneo bunge la Saku Guyo Bonaya, vijana wamaendelea kutumika vibaya katika mizozo hii kwani wanapatikana kwa urahisi. Bonaya ametaja kwamba Amani itapatikana kwa urahisi iwapo vijana watahusishwa kikamilifu katika safari kuzipatanisha jamii. Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya soka kwenye eneo hilo.
Baadhi ya vijana waliohudhuria hafla hiyo wamepongeza hazina ya CDF na kukariri kwamba wanafurahia kuweza kuunganishwa pamoja kwa jamii mbalimbali za Marsabit huku wakiwa na matarajio kuwa zoezi hilo litazidisha uwiano na utangamano kati yao. Aidha wametoa changamoto kwa viongozi katika eneo hilo kuwekeza katika mbinu zaidi za kuwaleta pamoja kama vile michezo.