Viongozi mbalimbali wameendelea kutuma jumbe za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa waziri wa elimu Prof. George Magoha aliyeaga dunia jioni ya jana katika hospitali ya Nairobi akiwa na umri wa miaka 71.

Kamishna mkuu wa uingereza nchini Jane Marriot amesema kuwa prof. Magoha atakumbukwa kwa kuwaunganisha wanafunzi wa humu nchini na wale wa uingereza sawa na kuendeleza uhusiano njema wa elimu kati ya uingereza na Kenya.

Wabunge pia kwa upande wao wamemkumbuka Prof. Magoha kwa mageuzi aliyoyaleta kwenye sekta ya elimu.

Wengi walimfahamu kama waziri ambaye alileta mageuzi katika sekta ya elimu humu nchini wakati ambapo sekta hiyo ilikuwa imekumbwa na changamoto si haba.

Prof George Albert Omore Magoha alizaliwa mwaka wa 1952 Katika kaunti ya Kisumu. Magoha alianza elimu yake ya msingi katika shule ya Yala na kuhamia Nairobi akiwa na umri wa miaka 6 baada ya kuanza kuugua ugonjwa wa pumu.

Alipokamilisha masomo yake ya msingi, Magoha alijiunga na shule ya wavulana ya Starehe na kisha baadaye Strathmore kwa elimu yake ya shule ya upili.

Magoha alipata ufadhili wa masomo ambapo alielekea katika chuo kikuu cha Lagos nchini Nigeria ambapo alisomea udaktari. Masomo yake yalimpeleka hadi katika chuo kikuu cha mafunzo huko Lagos, Chuo cha Ibadan na kisha chuo cha uzamifu wa daktari cha Royal nchini Uingereza.

Prof. Magoha alikuwa mtaalam wa masuala ya kiume. Mwishoni mwa mwaka wa tisini, Magoha aliteuliwa kuwa Mwenyekiti na mwalimu mkuu wa chuo cha mafunzo ya afya na kisha naibu wa chansela wa chuo kikuu cha Nairobi.

Mwaka wa 2016, aliteuliwa kama mwenyekiti wa baraza la kitaifa la mitihani KNEC ambapo alianzisha harakati za kukabiliana na udanganyifu na wizi wa mitihani ya kitaifa.

Harakati hizo za kupambana na waliohusika na sakata ya wizi wa mitihani zilimpa sifa tele ambapo tarehe 1 mwezi machi mwaka 2019 aliteuliwa kuwa waziri wa elimu chini ya serikali ya rais Uhuru Kenyatta na kuapishwa rasmi tarehe 26 mwezi huohuo.

Alishikilia wadhfa huo hadi baada ya uchaguzi wa mwaka jana. Prof. Magoha amemwacha mkewe Dkt. Babra Magoha pamoja na mwana wao Dkt.Michael Magoha.

 

January 25, 2023