Mudavadi Kindiki Gachagua

Siku moja baada ya maandamano ya upinzani yaliyoteka maeneo mengi ya taifa siku ya jana, viongozi mbalimbali serikalini wamejitokeza kukashifu machafuko yaliyoshuhudiwa kwenye maandamano hayo, ambayo kando na kusababisha hasara ya mabilioni ya fedha pia yalichangia vifo vya wananchi kadhaa huku wengine wakiendelea kupokea matibabu hospitalini. Leo, viongozi kadhaa serikalini wamejitokeza kukashifu maandamano hayo.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki, ameonya dhidi ya kushabikia uharibifu kama ulioshuhudiwa jana, akisema kuwa huenda hali hii ikalitumbukiza taifa katika matatizo mazito. Waziri Kindiki amesisitiza kwamba Wakenya wanafaa kutofautisha haki yao kikatiba na uhalifu kwa jina la siasa.

Kauli ya Waziri Kindiki imeungwa mkono na Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, ambaye amejitokeza na kukashifu vitendo vya upinzani, akisema kwamba serikali haitatishiwa na uharibifu au uhalifu wakati wa maandamano.

Mwingine aliyetoa hisia zake leo ni Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua, ambaye amemnyoshea kidole cha lawama kinara wa azimio, Raila Odinga, kwa vifo vilivyotokana na maandamano hayo. Gachagua aidha ameonya kuwa wale waliohusika na uharibifu katika eneo la Mlolongo na barabara ya Expressway watachukuliwa hatua.

 

July 13, 2023