Azimio

Viongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja katika kaunti ya Trans Nzoia wameahidi kuanzisha mchakato wa kukusanya saini kutoka kwa wananchi, ili kuwabandua wabunge waliounga mkono mswada wa fedha wa mwaka 2023.

Wakiongozwa na Eugine Wamalwa na mbunge wa Saboti Caleb Amisi, viongozi hao wamesema kwamba wakenya wana haki ya kusikilizwa, na hivyo uamuzi wa kuenda kinyume na sauti za wakenya waliowachagua unafaa kukataliwa vikali kote nchini. Amisi kwa upande wake aliinyoshea serikali kidole cha lawama, kwa kile alichokitaja kama nia ya kuwapunja wakenya katika mpango wake wa ujenzi wa makazi. Badala yake mbunge huyo ameitaka serikali kuwasaidia wananchi kulikabili tatizo la njaa.

Kuhusu maandamano ya upinzani yaliyopangwa kufanyika tarehe saba mwezi huu, Wamalwa amewahimiza Wakenya kujiandaa ili kushiriki katika maandamano hayo.

July 3, 2023