Kamukunji

Viongozi wa upinzani nchini wamewarai wakenya kuhudhuria mkutano wa mashauriano utakaofanyika jijini Nairobi wiki ijayo. Mkutano huo utakaoandaliwa katika uwanja wa Kamukunji siku ya Jumanne tarehe 27.06.2023 unapania kujadili hatua watakazochukua baada ya wabunge hio jana kuidhinisha Mswada wa Fedha.

Katika taarifa ya muungano huo iliyowasilishwa na Bi. Martha Karua siku ya Alhamisi, Viongozi wa Azimio wameikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kutojali kauli na kilio cha wakenya wakati wa kukusanya maoni ya umma kuhusu mswada huo, huku wakisema kuwa kutotiliwa maanani kwa maoni ya umma kunadokeza kuwepo kwa utawala wa kidikteta.

Upinzani umeshikilia kwamba mswada huo utawakandamiza wakenya wa kusababisha ongezeko maradufu la gharama ya maisha, hasa kipengee cha kuongeza Kodi ya VAT kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16. Bi. Karua katika taarifa yake aidha alieleza kuwa mkutano huo wa mashauriano utawapa wakenya nafasi ya kutoa maoni yao na kutafuta suluhisho mbadala kuhusu athari za Mswada huo.

June 22, 2023