CO27

Viongozi wa mataifa mbalimbali wanaohudhuria mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi wametoa mapendekezo juu ya hatua kali zinazotakiwa kuchukuliwa kudhibiti ongezeko la joto duniani.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley wamesema wakati umewadia kwa makampuni ya mafuta kuchangia katika hazina ya kuzisaidia kifedha nchi zinazokumbwa na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema mkutano huo unaofanyika mjini Sharm el-Sheikh nchini Misri, unapaswa kuweka mpango thabiti wa kuhitimisha utoaji wa gesi chafu.Wazo la kuyatoza kodi kubwa makampuni ya mafuta na gesi lilipata msukumo miezi ya hivi karibuni, ambapo makampuni hayo yamepata faida kubwa kutokana na kupanda sana kwa bei ya nishati, huku watumiaji wakitaabika kumudu kuweka joto majumbani mwao na kujaza mafuta kwenye magari.

November 8, 2022