Spika Wetangula

Shughuli za kawaida katika bunge la taifa alasiri ya leo, zilisitishwa baada ya kizaazaa kuibuka kuhusiana na uamuzi wa kumbandua Sabina chege kama naibu mnadhimu wa walio wachache katika bunge hilo.

Katika uamuzi wake, spika Wetangula alieleza bunge kwamba agizo la mahakama kuhusu mzozo unaoshuhudiwa katika chama cha Jubilee limemzuia kuidhinisha mabadiliko yoyote kuhusu uongozi wa muungano wa Azimio bungeni. Baadhi ya wabunge wa upinzani wakiongozwa na Mbunge Millie Odhiambo walipinga msimamo wa Spika kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa kuwafurusha kutoka kwenye vikao vya bunge.

Wabunge wengine waliochukuliwa hatua za kinidhamu katika vikao vya leo ni pamoja na Mbunge mteule Sabina Chege, Fatuma Mnyazi (Malindi), Catherine Omayo (Busia), Joyce Kamene (Machakos), Rosa Buyu (Kisumu) na Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang’.

Katika uamuzi wa uwatimua bungeni, Spika aliwaadhibu wabunge hao kama ifuatavyo:

Millie Odhiambo, Rosa Buyu, TJ Kajwang, na Sabina Chege watakuwa nje ya bunge kwa kwa wiki mbili

Fatuma Mnyanzi na Catherine Omanyo kwa siku 5

Joyce Kamene – atakosa vikao 2 vya bunge.

June 8, 2023