Waziri wa Ardhi, makazi na mipangilio ya Miji Alice Wahome, amesema kwamba waajiri wote watakaokosa kulipa ushuru wa nyumba watachukuliwa hatua kali za kisheria sawa na kupigwa faini.
Usemi wa waziri huyo unajiri siku moja baada ya mahakama kuu nchini kuharamisha ushuru huo wa nyumba. Mahakama kuu katika uamuzi wa kesi iliyowasilishwa kupinga sheria ya fedha ya mwaka 2023, ilitoa agizo la kusitishwa kwa ulipaji wa ushuru wa nyumba kwa misingi kwamba haujajikita katika sheria, hata ingawa agizo lenyewe litaanza kutekelezwa januari 10 mwaka ujao.
Katika taarifa kwa umma, waziri Wahome amewataka waajiri kuendelea kuwasilisha ushuru wa nyumba za bei nafuu kutoka kwa mshahara wa jumla wa mfanyakazi pamoja na mchango wa Mwajiri.