Zaidi ya familia 40,000 katika kaunti ya Nairobi zinazokabiliana na athari za mafuriko zitapokea msaada wa kifedha kutoka kwa serikali kuu ili kutafuta makao mbadala. Msaada huo wa kifedha wa shilingi 10,000 kwa kila familia, uliotangazwa siku ya Jumatatu na Rais William Ruto, utasaidia familia hizo katika kujenga tena maisha yao.
Kiongozi wa taifa, akiwa katika eneo la Mathare ambalo ni mojawapo ya maeneo mengi ambayo yameathirika na mafuriko, aliwahakikishia wahanga kuwa serikali iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.
Katika hotuba yake, Rais pia aliwahakikishia wananchi msaada wa vyakula na mahitaji mengine ya msingi. Zaidi ya hayo, rais alisisitiza kuwa mipango zaidi imewekwa ili kuhakikisha kwamba jamii zilizoathirika hazitafurushwa kutoka kwenye makao yao ya muda hadi watakaporejelea hali yao ya kawaida.
Kando na msaada wa moja kwa moja kwa familia, kiongozi wa taifa alieleza kwamba serikali pia imejitolea katika kurekebisha shule zilizoathirika. Jumla ya shilingi bilioni moja zitatumika katika kukarabati na kujenga upya shule zilizoharibiwa na mafuriko. Hadi kufikia sasa, wananchi wapatao 228 wamedhibitishwa kuaga dunia kutokana na mafuriko ambayo yanashuhudiwa nchini.