Sehemu ya viongozi wa upinzani wameapa kutohudhuria maandamano yaliyoratibiwa na muungano wa Azimio siku ya Jumatatu.

“Tunataka kusema kwa dhati kwamba hatutashiriki katika maandamano yaliyopangwa. Vile vile tunawasihi wapiga kura wetu kufanya vivyo hivyo. Tunawahimiza wale ambao watajiunga na maandamano hayo kurejea katika shughuli zao za kawaida za kiuchumi na kijamii haraka iwezekanavyo, hasa wale wanaojishughulisha na kilimo ili kufaidika na mvua inayonyesha kwa sasa kulima na kupanda,” Mbunge wa Suba Bw. Caroli Omondi

Viongozi hao wanaojumuisha wabunge Gideon Ochanda (Bondo), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Paul Abuor (Rongo), Elisha Odhiambo (Rongo), Felix Odiwuor Jalang’o ( Lang’ata) pamoja na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda wamewarai wabunge wenzao kususia maandamano hayo, wakieleza kwamba matatizo yanayolikabili taifa kwa sasa hayawezi kusuluhishwa kamwe kwa njia ya maandamano.

Wabunge hao wameeleza kwamba katiba ya Kenya inatoa fursa kwa mkenya yoyote kushiriki katika maandamano, ila wamewataka wananchi watakaoshiriki katika maandamano hayo yaliyoitishwa na kinara wa Muungano wa Azimio la umoja Raila Odinga, kufanya hivyo kwa njia ya aman.

Viongozi hao aidha wameeleza Imani yao kwamba mwafaka utapatikana kati ya pande zote husika.

March 17, 2023