Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya Mazingira duniani hii leo, wananchi na wafanyabiashara katika eneo la Ololulung’a chini ya makundi mbalimbali kama vile Mazingira Ammbassadors of Change, Elite Youth na Ololulung’a Pioneers walijihusisha katika shughuli mbalimbali za kuyalinda mazingira kama vile upanzi wa miti na kusafisha mji huo kwa kuzoa taka.
Akizungumza kwenye mahojiano katika kipindi cha DIRA YA KAZI mapema leo Bi. Judith Kirorei, ambaye ni naibu mwenyekiti wa wafanyabiashara eneo la Ololulung’a aliwarai vijana kuwa wazalendo na kujivunia juhudi za kuimarisha ubora wa mazingira, akisisitiza kwamba uzalendo ndio mwanzo wa safari ya kuyatunza mazingira.
Aidha Bi. Kirorei pia aliwataka wasafiri wenye hulka ya kutupa chupa za plastiki barabarani kujiepusha na uchafuzi huu wa mazingira, akieleza kwamba kando na kuwa hatari kwa mazingira pia, kuna uwezekano wa hulka hii kusabaisha ajali za barabani.
SAUTI: BI JUDITH KIROREI
Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani huadhimishwa kila siku ya tano ya mwezi Juni kwa madhumuni ya kutoa hamasisho kwa watu kuyalinda mazingira. Humu nchini kaunti mbalimbali, viongozi wa kisiasa na mashirika ya kijamii yalijihusisha katika maadhimisho haya kwa njia mbalimbali za kuboresha mazingira ya sasa na hata ya siku zijazo.
Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni kupambana na Uchafuzi unaotokana na Plastiki. #BeatPlasticPollution.