BY ISAYA BURUGU 17TH AUG 2023-Baadhi ya wafanyibiashara wa nafaka mjini Narok wamekiri kwamba bei ya bidhaa hiyo imeshuka kwa kiwango kikubwa  kwenye  sehemu nyingi katika  kaunti hii tangu msimu wa uvunaji  kuanza.Kulingana na Elizabeth Sironka mmoja wa wauzaji wa nafaka mjini Narok bei ya bidhaa nyingi za nafaka imepungua.

Amefichuwa kwamba zaidi ya miezi miwili iliyopita, walikuwa wanauza kila mkebe wa kilo 2 wa mahindi kwa shilingi 200 lakini kwa sasa baada ya wakulima wengi Narok kuanza kuvuna mahindi bei hiyo imepungua hadi shilingi 170 kwa mkebe.Vile vile ameongeza kwamba mkebe wa kilo 2 wa viazi ulikuwa unauzwa  shilingi 200 lakini kwa sasa unauzwa  shilingi 50.

Kwa upande wake Sharon Koina ambaye ni mfanyibiashara wa  hoteli anasema kwamba awali walikuwa wakinunua indi moja bichi  kwa shilingi 40 lakini kwa sasa bei ya bidhaa hiyo imeshuka kwani indi moja bichi linauzwa kwa shilingi 15.

Hali ni sawia pia kwa Alfred Nyamwea ambaye anafanya biashara ya mahindi lakini anasema bei ya mahindi huenda ikapanda baada ya wengi wa wakulima kupoteza mimea yao kutokana na kiangazi.

August 17, 2023