Wajumbe wa serikali na upinzani walikutana hii leo jijini Nairobi katika juhudi za kupanga ratiba ya mazungumzo.
Mkutano huo ulifuatia agizo la spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula aliyewataka viongozi wa Azimio na Kenya Kwanza kupanga Ajenda.
Uongozi wa bunge kutoka miungano ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza uliamua kuwachagua wabunge wa Rarieda Otiende Amolo na mwenzake wa Tharaka George Murugara kuongoza mazungumzo baina ya pande hizo mbili.
Wabunge hao wawili wataongoza kundi linalojumuisha seneta Ledama Ole Kina, Edwin Sifuna, Enoch Wambua, Amina Mnyanzi, Millie Odhiambo, mbunge David Pkosing (Azimio) na seneta Boni Khalwale.
Wengine ni pamoja na Hillary Sigei, Esther Okenyuri, Mwengi Mutuse, Adan Keynan, Lydia Haika kutoka (Kenya Kwanza).
Aidha wakati wa mkutano wa leo, pande zote mbili ziliibua wasiwasi kuhusu orodha ya wabunge walioteuliwa kuwakilisha pande zote mbili huku Azimio ukipinga kuteuliwa kwa Adan Keynan (Jubilee party) kwenye kamati hiyo,Kenya kwanza inapinga hatua ya Azimio kumteua David Pkosing (KUP) kama mwanachama wa kamati hiyo.