Wakenya wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na hatari ya kushuhudia mafuriko au maporomoko ya arthi wameagizwa kuhama kutoka maeneo yao. Hatua hii inachukuliwa kwa lengo la kuzuia hasara za mali na kuokoa maisha ya wananchi.
Katika taarifa ya Wizara ya Usalama wa Ndani, wananchi wanaoishi karibu na mabwawa 178 wameagizwa kutafuta makaazi mbadala katika kipindi cha saa 24 zijazo.
Jumla ya mabwawa 10 katika kaunti ya Narok yameorodhesha kati ya mabwawa hayo 178. Katika orodha hiyo, mabwawa matatu yametajwa kuwa na nyufa zinazoashiria hatari ya kutokea kwa mafuriko. Mabwawa yaliyotajwa ni pamoja na mabwawa ya Nairragei Enkare, Kikuyian, Nailogilog eneo la Narok Mashariki.
Mabwawa yaliyotajwa kuwa hatari katika kaunti ya Narok
Bwawa lingine lililoorodheshwa ni Chepares katika eneo la Narok Kusini. Vilevile mabwawa ya Nagwinyi, Inkorienito, Tepesonik, Intimigom na Kiloturi katika eneo la Transmara magharibi pamoja na bwawa la Abossi katika eneo la Transmara Mashariki pia yametajwa kama maeneo ya hatari kwa usalama wa wananchi.
TAZAMA ORODHA KAMILI HAPA CS_Kithure_Kindiki_Vacation_and_Evacuation_Orders_May_2,_2024
Wakati hayo yakijri, serikali imetangaza kuwa imeanzisha kambi 115 za wakimbizi wa ndani kwa ndani kwa ajili ya kuhifadhi familia ambazo zimepoteza makazi yao. Wizara ya usalama wa Ndani ilibainisha kuwa kambi hizo zimewekwa katika kaunti 19.
Serikali pia imeeleza imekusanya rasilimali za kusambaza chakula kwa jamii zilizoathirika. Takriban watu 196,296 wameathiriwa na mvua kubwa iliyosababisha vifo vya watu 210 kufikia sasa.