Walimu wa shule za upili nchini sasa wanalitaka Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini KNEC kuogeza malipo wanayopata wakati wa kusahihisha mitihani ya kidato cha nne ya KCSE.
Katibu mkuu wa Muungano wa Walimu wa shule za Upili (Kuppet) Akelo Misori amesikitikia hali duni ya mazingira ambayo walimu hao wanatekeleza majukumu yao, sasa akilitaka baraza la mitihani kupongeza malipo hayo kutoka kwa shilingi 55 kwa kila nakala ya mtihani inayosahihishwa hadi shilingi 100 kwa baadhi ya mitihani.
Katibu huyo amesema kuwa malalamishi haya ni baadhi ya maoni na kilio wanachopokea kutoka kwa walimu wanaoendeleza zoezi hilo kwa sasa katika shule mbalimbali kwenye kaunti ya Nairobi, akiahidi kuwa iwapo kilio chao hakitasikilizwa basi watasusia zoezi lijalo la usahihishaji wa mitihani hii.
Mapema leo, shughuli ya kusahihisha karatasi ya kwanza ya mtihani wa somo la dini katika shule ya upili ya Mangu, ilitatizika baada ya walimu kusitisha zoezi hilo na kuandamana wakilalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao na mazingira duni ya kazi, jambo ambalo Bw. Misori amelikashifu na kuitaka KNEC kuacha kutumia njia za kibepari katika zoezi la usahihishaji wa mitihani.
Kituo hicho cha shule ya upili ya St. Francis Girls eneo la Mangu kimefungwa na shughuli za usahihishaji kusitishwa kwa muda usiojulikana huku walimu waliokuwamo wakiondoka.