Wamiliki wa nyumba za kupanga mjini Narok wataanza kuwasajili wapangaji kama njia ya kukabiliana na uhalifu mjini Narok.

Kamishna wa Narok, Isaac Masinde, alitangaza haya siku ya Alhamisi, akisema kwamba itasaidia asasi za usalama kuwatambua wahalifu. Tangazo hilo limekuja baada ya soroveya mmoja kuuwawa usiku wa Jumanne 10.01.2024 eneo la K24 mjini Narok. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini mwake, Kamishna Masinde ameeleza kwamba baadhi ya wapangaji wamekuwa wakihusika katika vitendo vya uhalifu, na kuendelea kuwahangaisha wananchi pamoja na kuvuruga amani bila kutambulika.

Zaidi ya hayo Masinde amesema kwamba viongozi wa mitaa watahusishwa kikamilifu katika kufanikisha usajili huu, huku akitoa wito kwa wamiliki wa nyumba kushirikiana na maafisa wa usalama.

SOMA PIA: Mwanaume Mmoja Aangamizwa na Majambazi Eneo la K24, Narok

Aidha, wahudumu wa bodaboda pia wameshauriwa kujiunga na makundi ya waendeshaji wengine ili waweze kutambulika kwa urahisi. Hii ni hatua ya ziada katika kuhakikisha kuwa watu wanaohusika na huduma hii muhimu mjini Narok wanaweza kufuatiliwa kwa karibu na vyombo vya usalama.

Kufuatia ongezeko la visa vya utovu wa usalama mjini Narok tangu mwezi Disemba, serikali imechukua hatua za dharura ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria na kuanzisha operesheni ya usalama katika maeneo yote ya Narok mjini.

 

January 12, 2024