Rais William Ruto amefanya mabadiliko makubwa serikalini kwa kuteua makatibu wapya wa idara mbalimbali za serikali. Katika uteuzi huo, wandani wa kinara wa ODM Raila Odinga wamepata nyadhifa muhimu.
Jane Kare Imbunya ameteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Utumishi wa Umma, huku Regina Akoth Ombam akipewa Idara ya Biashara. Cyrell Wagunda Odede atahudumu katika Idara ya Uwekezaji wa Umma na Usimamizi wa Mali ya Umma.
Caroline Wanjiru Karugu, aliyewahi kuwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyeri, sasa atasimamia Idara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame, na Maendeleo ya Kimaeneo.
Ouma Oluga, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa KMPDU, ameteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Huduma za Afya, akichukua nafasi ya Harry Kimutai.
Ahmed Abdisalan Ibrahim sasa atasimamia Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Kitaifa, huku Judith Naiyai Pareno akisimamia Idara ya Haki, Haki za Binadamu na Masuala ya Katiba. Bonface Makokha ameteuliwa Katibu wa Idara ya Mipango ya Kiuchumi.
Profesa Abdulrazak Shaukat sasa ni Katibu wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi, huku Stephen Isaboke akipewa Idara ya Utangazaji na Mawasiliano. Michael Lenasalon atahudumu katika Idara ya Ugatuzi, na Fikirini Katoi Kahindi atasimamia Idara ya Masuala ya Vijana.
Carren Ageng’o Achieng ameteuliwa katika Idara ya Maslahi ya Watoto. Aden Abdi Millah naye ameteuliwa katika Idara ya Uchukuzi wa Majini na Shughuli za Majini.
Mabadiliko Zaidi ya Makatibu Serikalini
Katika mabadiliko ya hivi punde, Rais Ruto pia amebadilisha baadhi ya makatibu waliokuwepo serikalini.
Aliyekuwa Katibu wa Elimu ya Msingi, Belio Kipsang, amehamishiwa Idara ya Uhamiaji, wakibadilishana na Prof. Julius Bitok.
Harry Kimutai amehamishiwa Wizara ya Madini, akichukua nafasi ya Elijah Mwangi, ambaye sasa atasimamia Wizara ya Michezo. Mwangi anamrithi Peter Tum, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Amos Gathecha amepandishwa kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, akitokea kwa Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma.
Waziri wa zamani wa Afya, Susan Nakhumicha, amerejea serikalini akiteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika UN-Habitat jijini Nairobi.
Majina ya wateule hao tayari yamewasilishwa bungeni kwa ajili ya kusailiwa kabla ya kuidhinishwa.