Majuma kadhaa baada ya Rais William Ruto kutangaza sera mpya ya kuruhusu wageni kutoka mataifa ya nje kusafiri nchini Kenya bila kuwa na Visa, kundi la kwanza la wasafiri wamefika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hii leo. Katika mfumo huu mpya wa usafiri, idara ya uhamiaji nchini inatoa idhini za kielektroniki kwa wasafiri walio na nia ya kusafiri kuja humu nchini.
Julius Bitok, Katibu wa Masuala ya Uhamiaji nchini, amethibitisha kuwa hadi kufikia siku ya Ijumaa 05 Januari 2023, idara hiyo ilikua imepokea jumla ya maombi 5000 ya usafiri bila Visa, huku maombi 2141 yakiidhinishwa.
Mpango huu wa visa bure ulitangazwa na Kiongozi wa Taifa mwaka jana, na lengo lake kuu ni kuimarisha mapato katika sekta ya utalii nchini. Sera hii inawapa wageni fursa ya kufurahia vivutio vyote vya kipekee vya Kenya bila vikwazo vya visa, hivyo kukuza ukuaji wa utalii na kuleta manufaa kwa uchumi wa taifa.