Washukiwa wanne wa mauaji ya mwanaharakati Eliud Chiloba wameachiliwa huru huku rafikiye Jacktone Odhiambo akifunguliwa mashtaka ya mauaji.
Hakimu mkuu wa mahakama ya Eldoret Richard Odenyo ameamuru Odhiambo ana kesi ya kujibu.
Aidha Bw. Odenyo amesema kuwa wanne hao walioachiliwa huru watatakiwa kuripoti katika ofisi za DCI mara moja kwa mwezi katika miezi mitatu ijayo.
Kwenye kesi nyingine ni kwamba maafisa wa upelelezi wameiomba mahakama kuwapa siku saba ili waendelee kumzuilia mwakilishi wadi wa Korogocho Absalom Odhiambo ili kutoa nafasi ya kukamilika kwa uchunguzi.
Odhiambo aliyefikishwa mahakamani mapema hii leo, anatuhumiwa kwa kosa la kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa muungano wa azimio la umoja katika uwanja kamkunji jijini Nairobi.
Hata hivyo, mawakili wake wakiongozwa na Danstan Omari walipinga ombi hilo wakisema kuwa Odhiambo si hatari na kwamba kushtakiwa kwake ni kisiasa.