Rais William Ruto afungua kasha la Mtihani wa Kitaifa katika shule ya msingi ya Kikuyu Township kaunti ya Kiambu

Watahiniwa milioni 1.2 wa Gredi ya Sita na wengine milioni 1.4 wa darasa la Nane, wameanza rasmi mitihani yao ya KPSEA na KCSE Mtawalia asubuhi ya leo. Maafisa wa wizara ya elimu nchini pamoja na maafisa wa kaunti wamekuwa katika maeneo mbalimbali ya taifa ili kuangazia jinsi shughuli hii inaendeshwa. Wasimamizi wa vituo mbalimbali vya mitihani walijitokeza katika masanduku ya kuweka mitihani hii asubuhi ili kupokea karatasi za mitihani hii kwa ajili ya vituo vyao.

Kiongozi wa Taifa Rais William Ruto Awaombea Watahiniwa Kiambu.

Kiongozi wa Taifa, Rais William Ruto, aliandamana na viongozi wengine serikalini akiwemo Waziri wa Elimu Eliud Machogu, Mkurugenzi Mkuu wa TSC Bi. Nancy Macharia, na Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi katika kusimamia zoezi hili katika shule ya msingi ya Kikuyu Township kaunti ya Kiambu. Rais alieleza dhamira ya serikali katika kuendeleza elimu kwa wanafunzi wote nchini na kuwatakia kila la heri watahiniwa wa mwaka huu. Vilevile rais aliwaombea wanafunzi wa shule hiyo na watahiniwa wengine sehemu mbalimbali za taifa wanbapoanza mitihani hii.

 

Musalia Mudavadi Azindua Zoezi la Mtihani Nairobi.

Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi aliongoza uzinduzi wa mitihani katika shule ya msingi ya St George’s jijini Nairobi. Mudavadi alisisitiza umuhimu wa uadilifu katika mitihani na jinsi inavyosaidia kuandaa wanafunzi kwa maisha yao ya baadaye. Vilevile, alieleza matumaini ya kupata matokeo mazuri katika mitihani hii, hasa mtihani wa KCPE ambao utakuwa wa mwisho chini ya mfumo wa elimu wa 8-4-4.

Mwanafunzi Mmoja Kufanya Mtihani Hospitalini – Narok.

Katika kaunti ya Narok, zoezi hili lilizinduliwa rasmi na Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Bwana Apollo Apuko. Bw. Apuko alieleza kwamba Vituo 831 vya mitihani vya KCPE na vituo 922 vya KPSEA katika kaunti ya Narok vimejiandaa kuwahudumia watahiniwa. Hata hivyo, mwanafunzi mmoja kutoka eneo la Olulung’a, Narok Kusini, atafanya mtihani wake hospitalini akiwa mjamzito.

October 30, 2023