Watu wawili wameaga dunia katika ajali mbili tofauti za barabarani katika Kaunti ya Narok, chini ya saa 24 zilizopita.

Ajali ya kwanza ilitokea eneo la Tegero, Ololulung’a Narok Kusini, saa saba na robo usiku wa kuamkia Jumatatu 08.01.2023, na ilihusisha matatu aina ya Toyota Hiace inayomilikiwa na Kampuni ya Transcar Galaxy Sacco na Lori aina ya Mitshubishi Fuso. Matatu hiyo iliyokuwa na abiria 16 ilikuwa ikielekea Narok ikitokea Bomet, kabla ya kugongana ana kwa ana na lori hiyo iliyopoteza mwelekeo.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi kutoka kituo cha Ololulung’a  dereva wa matatu hiyo aliaga dunia papo hapo, watu 5 wakapata majeraha mabaya, huku wengine 11 walipata majeraha madogo. Dereva wa lori hilo hata hivyo hakuathiriwa katika ajali hiyo.

Katika ajali ya pili, mwendeshaji wa pikipiki mjini Narok aliaga dunia papo hapo baada ya kugongwa na basi katika eneo la KimsBreeze mjini Narok siku ya Jumapili 07.01.2023.

OCPD wa Narok ya Kati John Momanyi, amesema basi hilo na mwendeshaji huyo wa pikipiki walikuwa wakielekea Narok Mjini kabla ya mwendeshaji wa pikipiki aliyekuwa mbele ya basi kuteleza na kuanguka katikati ya barabara. Juhudi za dereva wa basi kusimamisha basi hilo hazikufanikiwa, na hivyo kumgonga na kufariki papo hapo.

 

January 8, 2024