Watu wawili walioshtakiwa kwa mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara watasalia rumande kwa siku 21 huku polisi wakifanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Washtakiwa wawili Brian Kimutai Bepco, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara na John Mwangi Kashu walitajwa kuwa washtakiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo kwani walikuwa watu wa mwisho kuonekana wakiwa na marehemu katika eneo la burudani mjini Narok.
Wakili Mkuu Mwandamizi wa Mashtaka ya Narok, Duncan Ondimu kutoka idara ya mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aliambia mahakama kuwa marehemu Adah Nyambura aliripotiwa kutoweka katika Kituo cha Polisi cha Narok mnamo Aprili 30, 2023 asubuhi na jioni mwili wake uligunduliwa katika eneo la Macedonia viungani mwa mji wa Narok.
Ripoti ya awali ilionyesha kuwa marehemu alibakwa kabla ya kuuawa. Mwili huo ulipelekwa katika makafani ya Hospitali ya Rufaa ya Narok ambapo uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanyika Mei 1, 2023, na sampuli muhimu zilitolewa kwa madhumuni ya uchunguzi wa kitaalamu.
Ondimu alisema kuna haja ya kuwahoji mashahidi kadhaa ambao walimwona marehemu kabla ya kukutana na kifo chake cha kutisha, ambao wengi wao ni wanafunzi wa chuo hicho.
Afisa mpelelezi Koplo Richard Simuyu alisema walalamikiwa wawili huenda wakahitilafiana na ushahidi iwapo wataachiliwa kwa dhamana.
Koplo Simuyu aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza (Brian), awali alisimamishwa shuleni kwa makosa ya kinidhamu na Chuo Kikuu cha Maasai Mara na kukutwa na simu ya mkononi ya marehemu.
Alisema simu ya mkononi ya marehemu na ya washtakiwa hao wawili zitafanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika makao makuu ya DCI.
Walipoulizwa kuhusu maoni yao kuhusu ombi lililotolewa na waendesha mashitaka, washtakiwa hao hawakuwa na majibu, na hivyo kuilazimu mahakama hiyo kuridhia ombi lao la kuwazuilia.
Kesi hiyo itatajwa Mei 23, 2023.