Mishahara ya wafanyakazi wa umma wakiwemo walimu, maafisa wa polisi, na wafanyakazi wengine wanaotekeleza majukumu yao katika ofisi za umma inatarajiwa kuongezeka kwa kati ya asilimia 7-10 kuanzia hapo kesho.

Haya ni kwa mujibu wa Rais William Ruto ambaye amesema kwamba ongezeko hili la Mishahara linatokana na hali ya sasa ya gharama ya maisha humu nchini. Akizungumza kutwa ya leo wakati wa uzinduzi wa mtandao wa utoaji wa huduma za serikali nchini, Rais amesema kwamba viongozi wa serikalini kuanzia kwa ofisi yake hadi kwa wabunge watasalia na mishahara yao wanayopokea sasa, huku akiiagiza tume ya kuratibu mishahara ya umaa kuangazia njia bora zaidi za kupunguza pengo la mishahara kati ya maafisa wa serikali na wafanyakazi wengine serikalini.

Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma za serikali, Rais William Ruto ameeleza kwamba  kila huduma ya serikali inayolipiwa itakua inalipiwa kwenye mtandao wa E-Citizen. Rais aidha ametoa amri ya kufungwa kwa nambari za malipo (Paybill) zinazotumika kufanya malipo ya huduma za serikali na kuhakikisha kwamba huduma zote za serikali zinatumia nambari moja ambayo ni 222 222, huku akiiagiza mamlaka ya ukusanyaji ushuru KRA kuimarisha mitambo yake ili kuweza kukusanya ushuru kwa njia ya kidijitali.

June 30, 2023