Magari

Wauzaji wa magari yaliyotumika sasa watalazimika kuwa waangalifu na kuepuka kutoa taarifa za uongo kwa wanunuzi wao, kwani wanaweza kushtakiwa na kuwajibishwa kisheria. Hii ni kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, uliothibitisha kuwa wauzaji hawawezi kujiondoa kwenye dhima ya uwakilishi mbaya, hata wanapouza magari chini ya makubaliano ya As is where is.

Uamuzi huo ulitolewa katika kesi dhidi ya kampuni ya Best Cars Limited (Impact Motors), iliyoshtakiwa na wanunuzi Morara Omoke na Esabel Gathigia baada ya kununua gari aina ya Volkswagen Golf kwa shilingi 630,000 mnamo Januari 2020.

Wanunuzi hao waliieleza mahakama kuwa muuzaji wa gari hilo aliwahakikishia kuwa gari hilo lilikuwa katika hali nzuri, lakini lilianza kupata matatizo ya kiufundi, mara baada ya kulinunua. Walalamishi hao walieleza kwamba walilazimika kutumia shilingi 400,000 zaidi kulikarabati gari hilo na wakaamua kumshtaki muuzaji kwa uwakilishi mbaya, wakidai kuwa taarifa kuhusu hali ya gari na maili yake zilikuwa za uongo.

Mahakama ya kutatua mizozo midogo iliwapa ushindi wanunuzi hao na kuwaamuru walipwe shilingi laki nne kama fidia. Muuzaji  kwenye kesi hiyo alikua amekata rufaa, lakini Mahakama Kuu, chini ya Jaji Linus Kassan, ilishikilia uamuzi huo na kutupilia mbali rufaa hiyo. Jaji Kassan alieleza kuwa wanunuzi hawawezi kutegemewa kuwa mafundi wa magari na kwa hivyo hawakuwa na uwezo wa kugundua kasoro zilizofichwa wakati wa ununuzi.

Kufuatia uamuzi huu, wauzaji wa magari yaliyotumika sasa watatakiwa kuwa waangalifu na kuhakikisha uwazi katika biashara zao, kwani utoaji wa taarifa za uongo unaweza kuwaweka katika hatari ya kushtakiwa na kulazimika kulipa fidia.

February 24, 2025

Leave a Comment