Wazee wa jamii ya Maa kutoka eneo la Ewaso Kedong, Kaunti Ndogo ya Kajiado Magharibi, wameelezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa visa vya uchinjaji haramu wa punda katika eneo hilo. wakizungumza kwenye kikao kilichoandaliwa na shirika la Farming Systems Kenya kwa ufadhili wa Brooke East Afrika, wazee hao waliitaka serikali kuchukua hatua za haraka ili kukomesha shughuli hizo haramu ambazo zimekuwa zikishamiri licha ya kupigwa marufuku.
Wazee hao wamesema kuwa punda wengi hununuliwa kutoka maeneo mbalimbali na kuchinjwa kinyume cha sheria katika Ewaso Kedong. Joseph Ndiambut, mmoja wa wazee wa kijiji katika eneo hilo, alitoa wito kwa wanajamii kutoruhusu ardhi yao kutumika kwa shughuli hizo haramu. Ndiambut alisisitiza madhara ya zoezi hilo kwa mazingira na hata kwa jamii. Wazee wa jamii hiyo walisema kwamba punda ni mnyama mtakatifu anayewasaidia katika shughuli mbalimbali.
Inspekta Peter Kobia, afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha eneo hilo, ameahidi kushirikiana na wanakijiji kukabiliana na biashara hiyo ambayo inatekelezwa nyakati za usiku. Inspekta Kobia pia alikiri kwamba kuna changamoto za kukabiliana na visa hivi. Changamoto hizi ni kama vile ukosefu wa gari la kushika doria ili kuwawinda watu wanaoendeleza shughuli hizi.
Shirika la Farming Systems Kenya limeelezea masikitiko yake kutokana na kuongezeka kwa uchinjaji wa punda, licha ya kuharamishwa kote nchini. Kulingana na FSK, zaidi ya punda 70 huchinjwa katika eneo hilo kila wiki, hali inayohitaji hatua za dharura.