Waziri wa elimu nchini Ezekiel Machogu amewaonya wakuu wa shule zote nchini dhidi ya kuruhusu kuendelea kwa biashara zozote za kibinafsi katika mazingira ya shule.
Akizungumza alipojiwasilisha bungeni ili kujibu maswali ya wabunge, Waziri Machogu ameeleza kwamba ni haramu kwa wafanyabiashara kujihusisha na biashara za aina yoyote shuleni, akieleza kwamba baadhi ya walimu wamekuwa wakishirikiana katika kufanikisha biashara hizi.
Aidha ameeleza kuwa baadhi ya wanasiasa na hasa wabunge wamekuwa wakiunga mkono shughuli hizi, kwa kuruhusu matumizi ya fedha za maendeleo ya maeneobunge katika ujenzi wa maeneo ya kuendeleza biashara kwenye mazingira ya shule.