Waziri wa Utalii Alfred Mutua ameeleza kuwa serikali ya kitaifa inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 7 kwa ajili ya kulipa fidia kwa waathiriwa wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la usajili wa vijana katika Huduma ya NYS, uliofanyika katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi, Mutua ameongeza kuwa visa vya wananchi kuvamiwa na fisi vimeongezeka siku za hivi karibuni, hali inayotokana na kipindi cha ukame kilichoshuhudiwa nchini.
Waziri Mutua pia ametoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya uhifadhi wa wanyama pori kuepuka kutembea nyakati za usiku ili kujikinga na hatari zinazoweza kutokea. Taarifa ya waziri huyo imetolewa siku moja baada ya wanafunzi wa chuo kikuu cha MultiMedia kuandamana wakilalamikia kisa cha mwanafunzi mmoja wa chuo hicho kuvamiwa na fisi usiku wa Jumatatu 05.02.2024.
SOMA PIA:Alfred Mutua aomba wakenya kuwasaidia waathiriwa wa Tetemeko la Ardhi Uturuki.
Aidha, Waziri Mutua amebainisha kuwa serikali tayari imetangaza zabuni ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuweka ua katika mbuga mbalimbali nchini, hatua ambayo itasaidia katika kuzuia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.