Serikali ya Kaunti ya Narok imewataka wakazi kuwa waangalifu kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, ambayo imeongeza hatari ya mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.
Waziri wa Kukabiliana na Majanga katika kaunti hiyo, Bi. Josphine Ngeno, amesema wakazi wa maeneo ya karibu na mito na njia za maji wako katika hatari kubwa hasa katika maeneo ya Olmekenyu na Oltarakwa yaliyoko Narok Kusini.
“Watu wasijenge nyumba karibu na mito au kwenye njia ya maji, kwa sababu maji hayaombi ruhusa, bali yanawabeba watu,” amesema Waziri Ngeno akizungumza mjini Narok.
“Iwapo mtu anataka kuvuka mto na maji ni mengi, ni heri asubiri hadi maji yapungue.”
Idara ya Dharura Iko Tayari Kusaidia
Bi. Ngeno amesema kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati ya kukabiliana na dharura, ikiwemo kuwepo kwa nambari maalum ya dharura ambayo wananchi wanaweza kupiga simu na kusaidiwa kwa haraka.
“Tunawaomba wananchi wote wawe waangalifu. Kama serikali ya kaunti tuko na idara ya dharura, na tuko na nambari ya simu ambayo ukipata tatizo unaweza piga na utaweza kusaidiwa,” aliongeza.
Mvua Kubwa Yaendelea Kunyesha
Wito wa Waziri Ngeno unajiri wakati ambapo Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari ya mvua kubwa inayotarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi kwa juma moja lijalo.
SOMA PIA: Narok Yajiandaa Kumkaribisha Rais Ruto kwa Ziara ya Maendeleo ya Siku Mbili
Katika kaunti ya Narok, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupokea zaidi ya milimita 100 za mvua, huku maeneo mengine yakipokea kati ya milimita 20 hadi 50.
Increased rains next week as well https://t.co/6TSYSGjbu7 pic.twitter.com/LL9bkSpeKl
— Kenya Met Department 🇰🇪 (@MeteoKenya) April 8, 2025