Wizara ya Afya imethibitisha kisa cha tatu cha Mpox nchini, ambapo mgonjwa wa kike mwenye umri wa miaka 30 jijini Nairobi amepatikana na ugonjwa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth alitangaza Ijumaa kwamba mgonjwa huyo ambaye ana historia ya kusafiri hivi majuzi kwenda Uganda, kwa sasa yuko katika hali nzuri na anapokea matibabu katika kitengo cha kutengwa katika mji mkuu Nairobi.

Kisa hiki cha hivi punde kinafanya jumla ya visa vilivyothibitishwa vya Mpox nchini Kenya kufikia vitatu, kufuatia kugunduliwa kwa visa vingine viwili katika kaunti za Taita Taveta na Busia.

Hadi sasa, Wizara imepima jumla ya sampuli 89 za Mpox, huku 79 zikiwa hazina virusi hivyo na saba bado zinaendelea kufanyiwa uchambuzi.

Dkt Amoth alisisitiza kuwa Wizara ya afya imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali hiyo na imeongeza juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

August 30, 2024