Wizara ya Elimu inapania kuanzisha matumizi ya bayometriki shuleni. Kulingana na mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari KESSHA Kahi Indimuli, njia hiyo mpya ya kuwatambua wanafunzi itafuatilia mienendo yao.
Akizungumza wakati wa Kongamano la 46 la Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya mjini Mombasa, Indimuli alisema walimu na wazazi wengi wamekosoa matumizi ya namba za Mfumo wa Kitaifa NEMIS na kuiomba serikali kutafuta njia mbadala.
Aliitaka wizara hiyo kupitisha takwimu katika mfumo wa biometrics ambao upo shuleni na kuziunganisha katika mfumo huo mpya.
Haya yanajiri baada ya Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kufichua kuwa kwa muda zaidi ya wanafunzi 200,000 katika shule za upili hawajapata masomo.
Alihusisha hili na maelezo ya wanafunzi kutonaswa vya kutosha katika NEMIS.Machogu alisema hali hii inaweza kuendelea kwa muda hadi maelezo ya wanafunzi hao yatakaponaswa kikamilifu na kwa usahihi.