Mtu mwenye ugonjwa wa macho mekundu

Katibu katika wizara ya afya Mary Muthoni amethibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa macho mekundu au almaarufu (conjutivitis/Red eye Disease) katika Kaunti ya Mombasa.

Katika taarifa iliyochapishwa na wizara ya afya siku ya Alhamisi, Katibu huyo wa idara ya afya ya Umma na viwango vya kitaaluma, amesema kuwa ugonjwa huo unaosababishwa na bakteria husambaa kwa mtu baada ya kutagusana na mtu anayeugua tayari.

Ugonjwa wa Macho mekundu au conjutivitis husababisha macho kufura na rangi yake kuwa nyekundu. Macho pia huwa na majimaji na pia kuwasha unaosababisha watu kujikuna. Wakati mwingine wanaougua wanaweza kutokwa na matongo meupe au ya manjano.

Katika taarifa yake Bi. Muthoni amewataka wananchi kudumisha viwango vya juu vya usafi, kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima na kujitenga kwa wale wanaoshuku kuwa wameambukizwa, huku pia akitoa wito kwa wananchi kutafuta msaada wa wataalamu iwapo wanapata dalili zozote za ugonjwa huu.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Afya ya Umma Kaunti ya Mombasa, Dr. Khadijah Shikelly, ametoa wito sawia kwa wananchi kuimarisha usafi wa mikono ili kuzuia kuenea kwa Ugonjwa huu. Dr. Shikelly pia alisisitiza umuhimu wa kudumisha usafi wa mikono na kuepuka kutumia vifaa vilivyotumiwa na watu wanaougua.

SOMA PIA: Mahakama ya Rufaa yasitisha maagizo yaliyosimamisha utekelezaji wa SHIF.
January 25, 2024