Zaidi ya wanafunzi milioni 2.5 wa darasa la nane na sita mtawalia wameanza rasmi mtihani wao wa kitaifa ambao utakamilika siku ya jumatano.
Kati ya watahiniwa hao milioni 2.5, milioni 1.2 wanaadika mitihani ya KCPE huku 1.3 wakiwa wa kwanza kufanya mitihani ya KPSEA, chini ya Mtaala mpya wa CBC.
Maafisa wa Wizara ya Elimu walisambazwa katika vituo tofauti kusimamia mitihani hiyo.Watahiniwa wa darasa la nane hivi leo wameandika mitihani ya masomo ya Hisabati, Kiingereza na somo la kuandika la kiingereza huku Wenzao wa darasa la sita wakifanya Hisabati na Kiingereza.
Wakati huohuo kaunti kamishna wa Narok Isaac Masinde amesema kuwa asasi za usalama katika kaunti hii ziko imara kuhakikisha kuwa mitihani ya KCPE na KPSEA inaendelea bila changamoto zozote.
Akizungumza baada ya kufungua rasmi mitihani hiyo, Masinde ametoa hakikisho kuwa hakutakuwa na udanganyifu wa aina yoyote wakati wa mitihani hiyo huku akiwaonya wasimamizi wa mitihani dhidi ya kutumia simu za rununu kwenye vituo vya mitihani.
Kando na hayo, Masinde ameeleza kuwa jumla ya watahiniwa 70,762 wanafanya mitihani hiyo huku akiweka wazi kuwa mikakati dhabiti imwekwa kuhakikisha watahiniwa 248 ambao ni wajawazito wanafanya mitihani yao bila tashwishi yoyote.